Collector
Giriş Yap
Kenya kuandaa kongamano la kwanza kuhusu masuala ya bahari barani Afrika | Collector
Kenya kuandaa kongamano la kwanza kuhusu masuala ya bahari barani Afrika

Kenya kuandaa kongamano la kwanza kuhusu masuala ya bahari barani Afrika

KENYA itakuwa taifa la kwanza barani Afrika kuandaa kongamano la kimataifa la masuala ya baharini almaarufu Our Ocean Conference , litakalofanyika kati ya Juni 16 na 18 katika kaunti za Mombasa na Kilifi. Kongamano hilo la 11 litahusu uhifadhi wa bahari, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uwekezaji katika uchumi wa baharini. Likiongozwa na kaulimbiu “Bahari Yetu, Urithi Wetu, Mustakabali Wetu,” kongamano hilo linatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi wa dunia, wafanyabiashara, wataalamu wa sayansi na wanaharakati wa mashirika ya kiraia ili kujadili hatua za kulinda mazingira ya bahari na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi. Mkurugenzi Mkuu wa East African Wildlife Society (EAWLS), Nancy Ogonje, alisema kongamano hilo litakuwa mojawapo ya majukwaa muhimu zaidi duniani yanayolenga kulinda bahari. “Umuhimu wake ni kwamba litawasukuma wadau kutoa ahadi za utekelezaji, uwekezaji na mageuzi ya sera zinazolinda mifumo ya ikolojia ya bahari huku zikifungua fursa za kiuchumi,” alisema Ogonje. Kwa karne nyingi, Bahari ya Hindi imekuwa mhimili muhimu wa biashara, utamaduni na utalii nchini Kenya. Leo, uchumi wa baharini umeendelea kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta za uvuvi, usafiri wa baharini, utalii wa pwani na nishati inayotokana bahari. Katibu Mkuu katika Wizara ya Uchumi wa baharini Betsy Njagi, alisema kuandaa kongamano hilo kutaiweka Kenya kama kitovu muhimu cha mijadala ya kimataifa kuhusu masuala ya bahari na mazingira. Alisema sekta ya uchumi wa baharini huchangia takriban asilimia 2.5 ya Pato la Taifa (GDP), ikiwa na thamani ya zaidi ya Sh178.8 bilioni kila mwaka. “Ingawa mchango huo bado uko chini ya wastani wa kimataifa, sekta hii ni muhimu kwani inategemewa na mamilioni ya wananchi kupitia uvuvi, utalii wa pwani na usafiri wa majini,” alisema Njagi.

Go to News Site