Kinaya cha marehemu Raila kupewa heshima za urais alionyimwa akiwa hai

Kinaya cha marehemu Raila kupewa heshima za urais alionyimwa akiwa hai

KILIKUWA kinaya kwamba baada ya kifo chake aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, alipewa mapokezi na heshima za kijeshi zinazopewa walioshikilia wadhifa wa urais pekee, afisi iliyomkwepa mara tano. Gari maalum la kubeba silaha likiendeshwa na maafisa wa Jeshi la Ulinzi Nchini (KDF) lilifika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kupokea mwili wake. Jeneza lililofunikwa kwa bendera ya Kenya, lilipokelewa na Rais William Ruto, mjane wa Bw Odinga, Ida, na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta katika uwanja huo. Kwa heshima yake, ndege ya Shirika la Ndege Nchini (KQ) iliyobeba maiti yake kutoka Mumbai, India, ilipewa jina la RAO001. Maelfu ya waombolezaji waliofika katika uwanja huo wa JKIA walilia kumpoteza kiongozi huyo waliyemrejelea kama Baba. Katika majengo ya bunge, maafisa wa KDF walifanya maandalizi ya kuupokea mwili huo kwa ajili ya kutazamwa na umma. Lakini baadaye, waombolezaji walifurika katika majengo hayo na kuzua vurugu hali iliyolazimu serikali kuhamisha shughuli ya kutazama mwili hadi uwanja wa Kasarani. Hadhi ya kulazwa kwa mwili katika majengo ya bunge kutazamwa na umma, imewahi kupewa marais wa zamani pekee. Wao ni Daniel Moi na Mwai Kibaki, waliofariki Februari 2020 na Aprili 21, 2022, mtawalia. Mnamo Jumatano, Rais Ruto alitangaza kuwa Bw Odinga atapewa Mazishi ya Kitaifa na heshima zote husika. Usalama pia uliimarishwa katika hifadhi ya maiti ya Lee, ambako mwili ulitarajiwa kuhifadhiwa. Baadhi ya waombolezaji walikuwa wafuasi wake sugu, ambao kwa miongo kadhaa wamempigia kura katika majaribio yake matano ya kuingia Ikulu. Licha ya kupoteza katika chaguzi za urais mara tano, Bw Odinga ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali za marais Moi, Kibaki, Kenyatta na sasa Dkt Ruto. Siasa zake za kutetea masilahi ya raia wa kawaida zilimfanya kupendwa na wengi haswa wale waliotengwa na serikali zilizopita zilizoshikiliwa na watu kutoka makabila mawili. Katika uchaguzi mkuu wa 2007, alikuwa mwaniaji aliyepigiwa upatu kushinda. Hata hivyo, alishindwa kwa kura chache na Bw Kibaki, matokeo ambayo Odinga na wafuasi wake waliyapinga. Ghasia zilizofuatia zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, uharibifu mkubwa wa mali na zaidi ya watu 400,000 kufurushwa kutoka makwao. Lakini baada ya kutiwa saini kwa Muafaka wa Maridhiano, Bw Odinga alitunukiwa wadhifa wa Waziri Mkuu. Mazungumzo yaliyochangia muafaka huo yaliongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan. Kwa mara nyingine katika uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Odinga alipigiwa upatu kushinda ikizingatiwa kuwa aliungwa mkono na Rais aliyekuwa akiondoka, Bw Kenyatta. Hata hivyo, alishindwa na Dkt Ruto kwa kura 233,000 pekee. Lakini mnamo 2024, Bw Odinga kwa mara nyingine alifikiana kisiasa na Dkt Ruto chini ya Serikali Jumuishi.